Mji wa Arusha ulianzishwa mwaka 1830 na baadae mwaka 1948 ulipandishwa hadhi na kuwa mamlaka ya mji wakati huo ukiwa na wakazi wapatao 5320. Mji huu ndio makao makuu ya mkoa wa Arusha ulipo kaskazini mwa Tanzania. Mwaka 1980 mji wa Arusha ulipandishwa cheo na kuwa manispaa na baadae mwaka 2011 ulifanywa kuwa jiji.
Mji wa Arusha una mandhari nzuri na yakuvutia kwani umejengwa chini ya Mlima Meru ambao ni mlima wa pili kwa urefu nchini Tanzania. Mji huu umejizolea umaarufu zaidi kwa kuwa umbali mfupi na hifadhi maarufu ulimwenguni kama vile Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro Crater, Tarangire, Ziwa Manyara na Mlima wa Volkano hai wa Oldoinyo lengai. Kwa kuzingatia haya mji wa Arusha umekuwa kitovu kikuu cha utalii nchini Tanzania. Kwa sasa mji wa Arusha ndio makao makuu ya jumuia ya Africa Mashariki na ndipo mahakama ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ilipo.
Mazingira na hali
ya hewa
Ijapokua mji wa Arusha upo katika eneo la kitropik karibu na Ikweta ambapo wengi wangelitarajia kuwe joto kali lakini hali ya hewa ya Arusha ni ya wastani yenye ubaridi na joto kiasi kufuatia kujengwa katika mwinuko wa mita 1400 kusini mwa Mlima Meru. Uoto wa asili Arusha ni wa kijani na wakuvutia sana. Maeneo mengi yazungakayo mji wa Arusha yanatumika kwa kilimo cha umwagiliaji na huko ndiko yalipo mashamba makubwa ya kahawa, mboga mboga na maua.
Majira ya mvua yamegawanyika mara mbili, mvua za vuli ambazo hunyesha kwa muda mfupi kuanzia mwezi wa Novemba hadi mwanzoni mwa mwezi Januari. Mvua za masika hunyesha kuanzia mwezi wa March hadi May na mwezi wa Juni hadi August ni kipindi cha baridi kali.
Wakazi wengo wa maeneo yazungukao mji wa Arusha hujishughulisha na Kilimo cha Ndizi, mahindi, maharagwe pamoja na aina tofauti za mbogamboga kama vile nyanya, matango, hoho, maharage mabichi na nyingine nyingi.